Halmashauri Wilaya ya Misungwi yaadhimisha sherehe za miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania bara mwaka 2024 kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya umma wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Akizungumza na Wananchi na Watumishi walioshiriki kufanya usafi katika maeneo ya Stendi ya Mabasi ya Misungwi, Soko kuu Misungwi pamoja na soko la jioni la Gwambina tarehe 9 Disemba 2024, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi amewataka na kuwasihi wananchi kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao na kudumisha amani, umoja na mshikamano wakati tukiadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika na kuwaonya wale watakaoendelea kupuuzia zoezi la usafi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Mhe. Samizi ameongeza kuwa maendelo yaliyopatikana tangu kipindi cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi hivi sasa yametendeka mengi sana ikiwemo Daraja la JPM, Shule za msingi na Sekondari, miradi ya maji, Vituo vya afya na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya iliyopo Iteja, pamoja na Barabara kupitia awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuna mabadiliko sana ambapo asilimia kubwa ya watu ni vijana ambao hawakushiriki harakati za uhuru mwaka 1961, ila wana wajibu wa kuitunza ili kuikabidhi kwa vizazi vijavyo Taifa likiwa salama katika shughuli za kimaendeleo na fursa mbalimbali zipatikanazo katika awamu ya sita.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya ya Misungwi Bw. Addo Missama pia ametumia fursa hiyo kuwasihii wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika juhudi za kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa safi ambapo kila mmoja anapaswa kujenga utamaduni wa kuhakikisha eneo lake linakuwa safi muda wote kitendo ambacho kinapunguza atahari za kupata magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu.
Naye Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Misungwi Bi. Elly Makala mara baada ya kushiriki shughuli za usafi amesema kuwa latika kuadhimisha miaka 63 ya uhuru Tanzania bara taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa wana jukumu la kuwashirikisha wananchi na kuwakumbusha kutoa ushirikiano katika kuzuia vitendo vya rushwa visitokee mapema ili kuwezesha kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo kwa ubora na viwango vinavyotakiwa kulingana na thamani ya fedha.
Wakati huo huo Diwani wa Kata ya Misungwi Mhe. Mganyizi Feruzi amesema kuwa ni jambo jema na la kupongeza kila mmoja kushiriki katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanzania bara ambapo amewasihi wananchi kutosubiri kuambiwa kuhusu usafi wa mazingira bvadala yake wafanye usafi kuwa sehemu yao ya maisha ili kuepuka magonjwa mbalimbali ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Baadhi ya Wananchi wa Misungwi akiwemo Bi. Mary Joseph na Bw. Abdalah Kisamba wameeleza namna ambavyo wameadhimisha siku ya uhuru wamesema kuwa miaka 63 ya uhuru maendeleo yaliyopatikana kipindi cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi hivi sasa yametendeka mengi sana ikiwemo ujenzi wa Daraja la JPM la Kigongo hadi Busisi, ujenzi wa Reli ya kisasi ya SGR, Ujenzi wa Jengo la ofisi za Halmashauri ya Wilaya, Shule za msingi na Sekondari, Vituo vya afya na Hospitali ya Wilaya pamoja na Barabara kupitia awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuna mabadiliko sana tofauti na kipindi cha nyuma ambapo barabara zilikua chache huduma za afya na Elimu zilikua mbali na makazi, umeme na maji yalipatikana sehemu za miji pekee.
Wilaya ya Misungwi imeadhimisha Sherehe za Uhuru mwaka 2024 kwa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya umma sambamba na kufanya Kongomano na mdahalo wa majadiliano ya Wananachi kuhusu maendeleo ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ufundi na maendeleo ya jamii Misungwi, ambapo maadhmisho hayo yalipambwa na Kauli mbiu ya Miaka 63 “Uongozi madhubuti na ushirikishwaji wa Wananchi ni msingi wa Maendeleo yetu"
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.